Habari Mpya

MGOGORO MZITO MIRATHI YA ALIYEKUWA MUASISI NA ASKOFU WA KANISA LA EVENGELIST ASSEMBLES OF GOD TANZANIA (EAGT)

Marehemu Dk. Moses Samuel Kulola.

HALI ni tete! Familia ya aliyekuwa muasisi wa imani ya kilokole nchini na Askofu wa Kanisa la Evangelist Assembles of God Tanzania (EAGT), marehemu Dk. Moses Samuel Kulola (83), inadaiwa kuingia kwenye mgogoro mzito wa usimamizi wa mirathi ya mali alizoziacha kiongozi huyo.
CHANZO?
Ilidaiwa kuwa gogoro hilo limekuja baada ya mtu mmoja kuibuka na kudai yeye ndiye msimamizi halali.
Kwa mujibu wa chanzo makini, baada ya mazishi ya marehemu Kulola miezi mitano iliyopita, familia ilikaa kikao na kufuata taratibu za mirathi kwa kuzingatia wosia wa marehemu  ambapo mjane wa marehemu, Elizabeth Kulola ndiye aliyetakiwa kuwa msimamizi.

Nyumba ya Marehemu Dk. Moses Samuel Kulola.
KATUNZI
Habari zinapasha kwamba wakati familia hiyo ikiwa katika msimamo huo ghafla aliibuka mtu aitwaye Florian Katunzi ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT City Center, Temeke jijini Dar na kudai kuwa ndiye mrithi wa mali kisheria kwani marehemu Kulola alimweka kuwa msimamizi.
Ilidaiwa kuwa, Katunzi alisema ana maandishi halali ya tamko na wosia wa marehemu mzee Kulola.
 TAHARUKI
Chanzo chetu kiliendelea kutiririka kuwa, wanafamilia walijikuta wakitaharuki na kupigwa butwaa kuhusu jambo hilo ambapo walimuomba Katunzi awaoneshe wosia huo lakini alikataa katakata na kuamua kuufikisha mahakama moja ya mwanzo ya jijini hapa.
Ilibidi familia ilivalie njuga suala hilo hasa wakitaka kuuona wosia huo mpya jambo ambalo walifanikiwa.
 
PINGAMIZI
Habari kutoka ndani ya familia ya marehemu Kulola zinasema kuwa baada ya kuuona wosia huo, Septemba 29, mwaka jana, wanafamilia hao waliweka rasmi pingamizi kwa kile kilichodaiwa kuwa, ulikuwa na makosa mengi, ikiwemo tofauti ya ukubwa wa mihuri iliyopigwa kwenye ukurasa wa kwanza na wa pili kutoka mwisho.


Mchungaji wa Kanisa la EAGT City Center, Florian Katunzi.
Pia familia ilibaini tofauti ya saini za marehemu Kulola katika kurasa mbili, uwepo wa mashahidi wakati wosia huo ukisainiwa, uwepo wa watu ambao hawahusiki na mirathi hiyo kama vile Msimamizi Mkuu wa Huduma ya Ushauri Kibiblia na Maombezi (BCIC), Askofu Sylvester Gamanywa.
Kubwa zaidi, ilielezwa kuwa familia ilibaini kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa katika mahakama ya mwanzo kinyume na sheria ya mirathi ya mwaka 1984 inayotoa mamlaka kwa  mahakama ya hakimu mkazi pekee.


Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Lusekelo Anthony ‘Mzee wa Upako’.


MZEE WA UPAKO
Hata hivyo, kabla patashika hilo kuchukua sura katika familia hiyo, Mchungaji Katunzi na Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Lusekelo Anthon ‘Mzee wa Upako’ nusu washikane mashati baada ya Katunzi kumfuata mwenzake akitaka rambirambi aliyoahidi kuitoa wakati wa kifo cha mzee Kulola.
Siku hiyo Mzee wa Upako aliahidi kutoa rambirambi ya shilingi milioni 15 akimzidi mwenzake, Mchungaji Joseph Gwajima aliyetoa shilingi milioni 10.
Inaelezwa kuwa,  Mzee wa Upako alikuja juu akimuuliza Katunzi kwamba anadai kama nani katika familia ya marehemu.
 
MJANE WA KULOLA
Akizungumza na waandishi wetu kwa majonzi huku akiangua kilio mara kwa mara nyumbani kwake, Capripoint jijini hapa, mke wa marehemu, Elizabeth alisema amemwachia Mungu mambo yote na kuongeza kuwa jambo hilo linamuumiza na kumfanya akumbuke enzi za uhai wa mume wake.
Alisema kuwa mumewe alimwambia akifa watu wengi waliokuwa karibu yake watamkimbia na marafiki kugeuka maadui hivyo hashangai kinachotokea sasa.



Mke wa marehemu.
Akizungumzia uhusiano kati ya Katunzi na marehemu Kulola, mama Kulola alisema marehemu hakuwa na uhusiano na Katunzi kiasi cha kufikia kumwamini katika suala nyeti la familia kama mirathi.
Mbali na hilo, mjane huyo alisema siku zote alikuwa akimfahamu Katunzi kama ndugu katika Injili na si vinginevyo.
 Katika kuchimba zaidi, ilibainika kuwa hata uongozi wa Kanisa la EAGT ulimpa Katunzi sharti la kuachana na jambo hilo mara moja au kama angeendelea alipaswa kuacha vyeo na uumini wake wake katika kanisa hilo.
Ilisemekana pia kwamba, Katunzi aliahidi kutekeleza lakini mwishowe aliapa mbele ya familia hiyo kuwa angeendelea na kesi hiyo hadi kieleweke.

KATUNZI ANASEMAJE?
Baada ya kulinyaka sakata zima, Risasi Jumamosi lilimbana Mchungaji Katunzi ambaye alijitetea kama ifuatavyo:
“Wewe njoo uchukue ‘document’ uandike, nilishatangaza hadi kwenye magazeti, njoo uchukue sasa sitaki kuongelea suala hilo.”

NINI HATIMA?
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni haikujulikana nini hatima ya suala hilo.

TUJIKUMBUSHE
Askofu Kulola alifariki dunia Agosti 29, 2013 katika Hospitali ya African Medical Investments (AMI) iliyopo Slipway jijini Dar es Salaam baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu na kuzikwa jijini mwanza.
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
Designed By